0


Wanajeshi wa Algeria wamewaua wapiganaji 7 na kumkamata mwingine mmoja katika operesheni tofauti karibu na mpaka wake na Libya na Mali.
Habari zinasema magari mawili yaliyokuwa yakijaribu kuvuka mpaka wa nchi hizo mbili kwenye eneo la Bordj Badji Mokhtar yaliharibiwa. Tangu kuzuka kwa ghasia kaskazini mwa Libya na Mali, Algeria imekuwa ikituma wanajeshi kwenye mpaka wa nchi hizo mbili ili kuzuia wapiganaji na uingizaji wa silaha.
========.
Habari kutoka shirika la habari la Libya zimesema uwanja wa ndege za kijeshi wa Mitiga ulioko mji mkuu wa Libya Tripoli umeshambuliwa na kusababisha vifo vya askari wawili. Ofisa wa Mitiga amesema hadi sasa hali ya majeruhi na kundi lililohusika na mashambulizi hayo havijulikani. Hadi sasa uwanja wa ndege huo haujafunguliwa.
Habari nyingine kutoka nchini humo zinasema mahakama ya Libya imeahirisha kesi ya maofisa waliokuwa kwenye serikali ya Muammar Gaddafi hadi tarehe Novemba 30 kwa ombi la wanasheria wa utetezi. Hakimu wa mahakama hiyo ameruhusu kuahirishwa kwa kesi hiyo ili kukamilisha ushahidi.
========.
Waziri wa afya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) Bw. Felix Kabange Numbi amesema nchi hiyo imefanikiwa kudhibiti kabisa maambukizi ya virusi vya Ebola wakati tukio jipya la ugonjwa huo halijaripotiwa kwa siku 42 hadi kufikia Jumamosi.
Hata hivyo DRC imeweka kikosi cha dharura cha matibabu ili kuzuia kurudi tena kwa ugonjwa huo.
========.
Msafara wa magari ya Umoja wa mataifa mjini Baghdad jana asubuhi ulikumbwa na mlipuko, lakini mlipuko huo haukusababisha kifo wala majeruhi. Taarifa iliyotolewa na Umoja wa mataifa inasema msafara huo wa magari matatu ulikuwa unatoka uwanja wa ndege wa Baghdad kuelekea eneo la ofisi za mashirika ya kimataifa. Watumishi wote wa Umoja wa mataifa waliokuwa kwenye msafara huo walifika kwenye eneo hilo salama, lakini gari moja liliharibiwa vibaya.
Mjumbe maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa nchini Iraq Bw Nickolay Mladenov ametoa taarifa akisema tukio hilo haliwezi kuuzuia umoja wa mataifa kuendelea kuisaidia Iraq na watu wake, na kusema ataisaidia serikali ya Iraq kuhakikisha wahusika wanafikishwa kwenye mikono ya sheria.
Ripoti ya hivi karibuni ya umoja wa mataifa inaonesha kuwa kwa sasa Iraq inakabiliwa na hali kukosekana kwa usalama kuliko ilivyokuwa katika miaka ya hivi karibuni, ugaidi na vurugu nyingine vimesababisha vifo vya watu zaidi ya elfu 5,500 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, na wengine zaidi ya 11,600 wamejeruhiwa.
===========.
Rais Barck Obama wa Marekani amethibitisha kuuawa kwa mmarekani aliyekuwa anashikiliwa na kundi la ISIS Bw. Peter Kassig. Taarifa iliyotolewa na ikulu ya Marekani inasema Rais Obama ameeleza kuwa Bw Kassig ameuawa kwenye kitendo cha kiovu na kundi ambalo dunia nzima inalihusisha na vitendo vya kinyama
Video moja iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii na kundi la ISIS inaonesha mtu mmoja aliyeficha sura yake amesimama karibu na kichwa cha Bw Kassig. Video hiyo pia inaoesha kinachoaminika kuwa ni kuchinjwa kwa wanajeshi kadhaa wa Syria waliokamatwa.
Bw Kassig ambaye pia alijulikana kwa jina la Abdul Rahman alikuwa anafanya kazi ya kujitolea kuwasaidia watu waliojeruhiwa katika mapambano nchini Syria. Yeye ni mmarekani wa tatu kuuawa na kundi la ISIS katika muda wa chini ya miezi mitatu.
=======.
Mkutano wa 9 wa wakuu wa kundi la nchi 20 uliomalizika mjini Brisbane, Australia umetoa taarifa ukitoa kipaumbele kwa ongezeko la uchumi wa dunia, kuboresha maisha ya watu na kuongeza nafasi za ajira.
Taarifa hiyo ya Brisbane inasema kasi ya kufufuka kwa uchumi wa dunia ni ndogo, ongezeko la uchumi haliwezi kuleta nafasi za kutosha za ajira, na bado kuna hatari za fedha na kisiasa.
Viongozi wa nchi za kundi hilo wamekubaliana kuongeza kasi ya ongezeko la pato la taifa GDP kwa asilimia 2 nyingine katika miaka mitano ijayo, na kusisitiza umuhimu wa uwekezaji hasa katika miundo mbinu ili kuhimiza ongezeko la uchumi na kuongeza nafasi za ajira. Viongozi pia wamekubaliana kutoa urahisi kwa biashara ya kimataifa na kuzidisha ushirikiano katika sekta ya nishati.
=======.
Viongozi waandamizi wa Russia na Oman wamewasili leo hapa mjini Tehran kwa ajili ya ziara rasmi ya kikazi.
Spika wa Bunge la Russia DUMA Bw. Sergey Naryshkin na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Bw. Yusuf bin Alawi waliowasili leo hapa Tehran, wanatarajiwa kuwa na mazungumzo na viongozi mbalimbali wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Spika wa Bunge la Russia amesema kuwa lengo la safari yake hapa nchini Iran ni kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika masuala mbalimbali yakiwemo pia masuala muhimu ya kimataifa.


Naibu Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, yaani Bunge la Iran Bw. Abou Tourabi Far na Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Kigeni ya Bunge la Iran, Bw. Alauddin Burujerdi ndio waliompokea Spika wa Bunge la Russia katika Uwanja wa Ndege wa Mehrabad hapa Tehran.


Katika upande mwingine, safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Bw. Yusuf Bin Alawi imefanyika hapa Tehran baada ya mazungumzo ya hivi karibuni ya nyuklia yaliyofanyika mjini Muscat Oman kati ya Iran na kundi la 5+1.

Post a Comment

 
Top