Zaidi ya miaka mitatu imepita sasa ambapo kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh linafanya jinai katika nchi za Syria na Iraq. Kundi la kigaidi la Daesh limekuwa likiuwa watu ovyo na kuwalazimisha wengine kuwa wakimbizi. Umoja wa Mataifa pia katika ripoti yake umebainisha kuwa kundi hilo la kigaidi limefanya jinai kubwa. Ripoti hiyo imetayarishwa kwa kutegemea mahojiano na mazungumzo yaliyofanywa na watu zaidi ya 300 walioshuhudia jinai hizo na pia wakaguzi wa haki za binadamu wa umoja huo.
Ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa ni ya kwanza ya aina yake kuwahi kutolewa ambayo inalituhumu kundi la Daesh kuwa limekuwa likifanya ukatili mkubwa dhidi ya raia. Ripoti ya Umoja wa Mataifa imebainisha pia kwamba, Daesh ni kundi lililoratibiwa ambalo linatumia ukatili na kuwatwisha raia sheria zake kwa ajili ya kutimiza malengo yake ya muda mrefu.
Mkuu wa Kamisheni ya Utafiti ya Umoja wa Mataifa Paulo Sérgio Pinheiroamesisiza kwamba, viongozi wa kundi la Daesh wametenda jinai dhidi ya binadamu kwa mpangilio kamili na kwa kujua wanalolifanya. Kwa msingi huo, Pinheiro ametoa wito wa kushtakiwa wakuu wa kundi la kigaidi la Daesh katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).
Katika miaka ya hivi karibuni Daesh haikusita kufanya jinai yoyote ile huko Syria na hivi sasa kundi hilo limepanua zaidi hujuma na ukatili wake nchini Iraq. Kuwakata watu vichwa, kuwafanya watumwa wa ngono, mauaji ya umati na kuwanyonga wanawake na wanaume hadharani ni sehemu ya jinai chungu nzima zinazofanywa na kundi la Daesh huko Syria na Iraq. Ni karibu miaka minne sasa ambapo wananchi wa Syria kila siku wanapaza sauti kuonyesha namna walivyodhulumika, lakini hakuna sikio linalosikia kilio chao hicho.
Nchi za Magharibi hususan Marekani ambazo leo hii zinadai kupambana na Daesh, ndizo hizo hizo ambazo zilikuwa zikilifadhili kifedha na kulipatia silaha kundi hilo la kigaidi na kitakfiri katika miaka yote ya mgogoro wa ndani nchini Syria. Ushahidi unaonyesha kuwa, makundi ya kigaidi yanayofanya ukatili na mauaji ya kutisha katika nchi za Iraq na Syria yameasisiwa na nchi za Magharibi kwa msaada wa baadhi ya nchi za Kiarabu.
Miaka iliyopita kundi la kigaidi la al Qaida lilihesabiwa kama tishio kwa dunia, lakini sasa makumi ya makundi mengine yamejitokeza kutokana na kundi hilo la kigaidi, ambapo Mkuu wa Kamisheni ya Utafiti ya Umoja wa Mataifa ametamka wazi kwamba, lengo la makundi yote hayo ni kuzusha hofu na wasiwasi na kueneza fikra za kitakfiri katika maeneo mbalimbali duniani.
Maeneo ya harakati za makundi ya kigaidi sasa yamepanuka zaidi kutoka Syria na Iraq hadi huko kaskazini mwa Afrika. Ansarul Sharia, Ansar Baitul Muqaddas na Ansar al Sunna, ni baadhi ya makundi ya kigaidi ambayo yamekuwa yakianzisha vita na kufanya jinai chungu nzima katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati.
Hadi sasa Umoja wa Mataifa ambao wajibu wake mkuu ni kulinda amani na usalama duniani umetosheka tu kwa kulaani kwa maneno matupu jinai na ukatili wa makundi hayo ya kigaidi na hatua za wadhamini na wasaidizi wao wa fedha na silaha. Hii ni pamoja na kuwa jumuiya hiyo ya kimataifa ingeweza kutumia uwezo wake kuzuia jinai za makundi hayo na washirika wao.
Hakuna shaka kuwa makundi ya kigaidi ni tishio kwa ulimwengu mzima. Lakini swali linalojitokeza ni kuwa nani mwenye makosa na wa kulaumiwa?
Ni wazi kuwa serikali nyingi za Ulaya na Marekani ambazo zimekuwa na nafasi katika kuibuka kwa makundi ya kigaidi, ndizo zinazopaswa kulaumiwa kutokana na jinai zote hizo dhidi ya binadamu zinazofanywa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh. Hii ni kwa sababu nchi hizo zimeshiriki pakubwa katika kuundika na kuimarika kundi hilo la kigaidi na mengine kama al Qaida japokuwa sasa makundi hayo yameondoka chini ya udhibiti wao na kuanza kuwauma hata mabwana na waanzilishi wao.
Post a Comment