
Wananchi wa Zambia wamejitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi wa
rais atakayechukua nafasi ya hayati Michael Sata ambaye alifariki dunia
mjini London mwezi Oktoba mwaka uliopita. Kumeripotiwa mvua kali katika
aghalabu ya maeneo ya Zambia lakini watu walijitokeza baadaye mchana
katika masanduku ya upigaji kura. Hali imeripotiwa kuwa ni shwari huku
uchaguzi ukifanyika kwa amani. Mgombea wa chama tawala cha Patriotic
Front (PF) Edgar Lungu mwenye umri wa miaka 58 na ambaye pia ni Waziri
wa Ulinzi kwa sasa ana matumaini ya kupata ushindi katika uchaguzi wa
leo. Licha ya kuweko wagombea kadhaa wanaowania kiti hicho, lakini
Hakainde Hichilema mgombea wa chama cha upinzani cha UPND anatajwa kuwa
mpinzani mkuu wa Edgar Lungu katika uchaguzi wa leo. Tume ya uchaguzi ya
Zambia imetangaza kuwa, zoezi la kuhesabu kura litaanza muda mfupi tu
baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika. Taarifa ya tume hiyo imeeleza
kuwa matokeo ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa katika kipindi cha
masaa 48. Mwangalizi mkuu wa uchaguzi kutoka Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika SADC Maite Nkoana Mashabane amepongeza kujitokeza
idadi kubwa ya wapiga kura ambao walikuwa na subira. . Hivi sasa nchi
hiyo inaongozwa na aliyekuwa makamu wa rais wa Sata, Guy Scott Mzambia
mzungu, ambaye kutokana na kwamba wazazi wake walizaliwa nje ya nchi
hiyo, amezuiliwa kugombea katika uchaguzi huo.
Post a Comment