Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, alitoa tamko hilo wakati akiwahutumia maelfu ya wananchi katika kilele cha sherehe za maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye Uwanja wa Amaan visiwani hapa jana.
Shein alisema uamuzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa azima ya Mapinduzi ya mwaka 1964 kama ilivyoagizwa Rais wa Awamu ya Kwanza, Abeid Amani Karume, Septemba 23, 1964.
Alisema tamko hilo litaanza kutekelezwa rasmi mwaka ujao wa fedha, Julai Mosi, mwaka huu.
“Kuanzia mwaka ujao wa fedha, serikali itachangia elimu ya msingi kwa maana kwamba wanafunzi hawatachangia elimu hiyo,” alisema Dk. Shein.
“Pia kwa upande wa sekondari, serikali italipia ada ya mitihani ya taifa kwa kidato cha nne na sita. Kuhusu ada malipo ya ada ya sekondari, serikali itatoa tamko baadaye,” alisema huku akishangiliwa na wananchi waliofurika kwenye Uwanja wa Amaan.
Wanafunzi wamekuwa wakichangia gharama za elimu ya msingi na sekondari wakilipa Sh. 5,000 na Sh. 10,000 (anapoanza) kwa shule za msingi, kuanzia Sh. 15,000 kwa ada ya shule za sekondari na Sh. 50,000 ikiwa ni ada ya mtihani wa taifa.
Dk. Shein alisema SMZ imeajiri walimu 1,781 katika ngazi mbalimbali ikiwa ni sawa na asimilia 74 ya mahitaji, hivyo kuna uhaba wa walimu 62 (asilimia 26).
Kabla ya kutoa tamko hilo, Dk Shein aliwataka wananchi wa Tanzania kudumisha amani na utulivu wakati wa kuipigia kura Katiba inayopendekezwa na uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Kiongozi huyo pia aliwataka wananchi wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutii sheria za nchi katika kusimamia maslahi ya nchi na Muungano.
“Ni wajibu wa viongozi wote wa serikali, wanasiasa, viongozi wa dini na viongozi wengine katika jamii kuhakikisha kuwa amani na utulivu inadumishwa, inaendelezwa na sheria za nchi zinafuatwa.
“Mapinduzi yetu na Muungano wetu ndizo nguzo zetu kubwa za maendeleo yetu na ndizo zitakazotufikisha kule dira zetu za maendeleo zinakotuelekeza,” alisema.
MATIBABU BURE
Ili kupunguza vifo vya mama wajawazito, Dk Shein alikumbusha juu ya utekelezaji wa uamuzi wake wa Mei 2012, kina mama wajawazito wakajifungue kwenye vituo vya afya na hospitali za serikali bila malipo.
“Ninawataka wafanyakazi wa vituo vya afya na wodi za wazazi za serikali, kutowatoza wazazi fedha zozote wanapokwenda kujifungua kwa njia ya kawaida au ya upasuaji. Huduma hizi zinapaswa kutolewa bure,” alisema.
Aliendelea kueleza kuwa idadi ya madaktari wazalendo walioajiriwa visiwani hapa imefikia 102 baada ya kuajiriwa madaktari wapya wazalendo 37 Novemba mwaka jana huku kukiwa na madaktari 40 wa kigeni kunakoifanya idadi ya madaktari wanaotoa huduma kuwa 142.
“Kwa mujibu wa Sensa ya 2012, daktari mmoja anatoa huduma kwa watu 9,708. Jitihada za kusomesha madaktari na wataalam wengine wa afya zinaendelezwa,” alisema.
KUKUA KWA UCHUMI
Dk. Shein pia alisema Pato la Taifa limeongezeka kutoka Sh. bilioni 942.3 mwaka 2010 Sh. bilioni 1.443 mwaka 2013 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 53 huku akifafanua kuwa uchumi wa Zanzibar umekua kutoka asilimia 6.4 hadi 7.4 katika kipindi hicho.
Alisema Pato la Mtu Binafsi limeongezeka kwa wastani wa asilimia 38 kutoka Sh. 778,000 mwaka 2010 hadi Sh. milioni 1.08 mwaka 2013.
WATALII 274,619 ZENJ
Dk. Shein alisema katika utekelezaji wa Mpango wa Utalii kwa Wote, idadi ya watalii wanaofika visiwani hapa imeongezeka kutoka watalii 132,836 mwaka 2010 hadi 274,619 mwaka jana, ikiwa ni ongezeko la asilimia 107.
Alisema serikali inaandaa sera ya urithi wa utamaduni itakayotoa muongozo wa matumizi bora ya urithi ili kuimarisha shughuli za utalii huku akieleza kuwa maeneo yote ya kihistoria, mambo ya kale na urithi wa utamaduni yaliyopo katika maeneo mbalimbali visiwani hapa yataendelea kuimarishwa.
UKIMWI
Kuhusu VVU na Ukimwi, Dk Shein alisema: “kiwango cha maambukizi kinaendelea kubaki kuwa asimilia 0.6 na idadi ya wagonjwa wanaopata huduma ya ARV’s imeongezeka kutoka wagonjwa 2,341 mwaka 2010 hadi wagonjwa 4,669 mwaka 2014, ikiwa ni sawa na ongezeko la asimilia 99.”
Dk. Shein pia aliwahimiza wananchi kuendelea kujitokea kuchangia damu ili kuimarisha upatikanaji wa damu salama kwa mahitaji ya wagonjwa.
Aidha, alipongeza jitihada za serikali yake ya Awamu ya Saba kwa kuimarisha na kuendelea kuimarisha huduma za maji, miundombinu ya barabara, usafiri wa anga na bandari, kilimo, nishati, ufugaji, uvuvi, utamaduni na michezo, mawasiliano, viwanda na biashara pamoja na mapambano dhidi ya athari za mazingira na unyanyasaji wa kijinsia.
Hotuba ya Dk. Shein ilitanguliwa na gwaride kutoka kwa vikosi vya ulinzi na usalama lililoongozwa na msiamamizi mkuu, Brigedia Jenerali Cyril Mhaiki, burudani za ngoma za asili kutoka Pemba, Gairo (Morogoro), Unguja Kaskazini A na wimbo maalum wa Miaka 51 ya Mapinduzi ulioimbwa na wasanii wa kizazi kipya.
Kabla ya kumkaribisha Dk. Shein kutoa hotuba, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alisema tangu kuanza kwa shamrashamra za maadhimisho ya Miaka 51 ya Mapinduzi Januari 2, mwaka huu, miradi ya maendeleo 45 imezinduliwa Unguja na Pemba ikigharimu zaidi ya Sh. bilioni 136.
Kileleni hicho cha maadhimisho hayo kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wakiwamo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.
Jakaya Kikwete na Marais Wastaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa na mkewe, Anna.
Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mohamed Gharib Bilal; Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda; Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad; Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda; Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho; mawaziri wakuu wastaafu, mawaziri wa Muungano na Zanzibar, maofisa waandamizi wa serikali zote, mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa.
Post a Comment