Tunapoelekea
kipindi hiki cha uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambao unatarajiwa
kufanyika tarehe 14 Disemba, 2014, kwa taarifa tulizonazo, katika baadhi
ya maeneo hapa nchini, kumejitokeza makundi ya vijana wanaopita katika
baadhi ya maeneo na kuwatishia watu waliojiandikisha kupiga kura
hususani wazee na wanawake kuwa, siku ya kupiga kura wasijitokeze na
endapo watajitokeza watafanyiwa vurugu.
Jeshi
la Polisi nchini, linatoa onyo kali kwa mtu yeyote au kikundi chochote
cha watu kutokujihusisha na vitendo vya vurugu, fujo ama vitisho
vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani wakati wa zoezi zima la
uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa.Hata
hivyo, Jeshi la Polisi katika mikoa yote limejipanga vizuri kwa
kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba
hakuna vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani vitakavyojitokeza wakati
wa kampeni na hata siku ya kupiga kura na pale ambapo vitajitokeza
vitadhibitiwa kwa haraka, na wahusika kukamatwa.
Aidha,
Jeshi la Polisi nchini, linawatoa hofu wananchi wote kwamba, ulinzi
umeimarishwa katika maeneo yote kipindi hiki chote cha kampeni za
uchaguzi wa serikali za mitaa na hata siku ya upigaji kura.
Waliojiandikisha kupiga kura wote wajitokeze siku ya kupiga kura bila
hofu ya aina yoyote.
Jeshi
la Polisi linaendelea kuomba ushirikiano wa jamii kutoa taarifa za mtu
ama vikundi vya aina yoyote vinavyojihusisha na vitendo vya vitisho,
vurugu na fujo dhidi ya wananchi waliojiandikisha kupiga kura ili hatua
kali za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao mapema.
Imetolewa na:-
Advera John Bulimba – SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Advera John Bulimba – SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.

Post a Comment