0
Amisi Tambwe kufunga goli lake la kwanza katika mechi yake ya kwanza kuichezea Yanga na Mrundi mwenzake Didier Kavumbagu kuitungua timu yake hiyo ya zamani, yalikuwa ni baadhi ya matukio yaliyogusa hisia katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara iliyomalizika kwa sare ya 2-2 dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Kocha Mholanzi Hans van der Pluijm aliyechukua mikoba ya Mbrazil Marcio Maximo aliyetimuliwa baada ya mechi yao iliyopita ya kirafiki ya Nani Mtani Jembe waliyolala 2-0 dhidi ya mahasimu wa jadi Simba, alianza na sare ambayo alisema ilitokana na makosa ya kimchezo.

"Mpira ni mchezo wa makosa. Tulicheza 4-4-2 na Azam walicheza 4-3-3 lakini tuliwaachia sana Azam wakatutawala katika eneo la kiungo. Tulifanya makosa katika kudhibiti wapinzani hasa katika goli la pili la kusawazisha la Azam. Tulimuacha John Bocco akiruka kufunga kwa kichwa peke yake bila ya upinzani," alisema Pluijm akuiongeza kwamba watayafanyia kazi mapungufu hayo. 

Kavumbagu aliifungia Azam FC bao la utangulizi baada ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga kuuwahi mpira uliopenyezwa ndani ya boksi na winga mpya Brian Majwega na kuwachanganya kipa Deogratius Munishi 'Dida' na mchezaji 'kiraka' Mbuyu Twite katika dakika ya sita ya mchezo huo wa raundi ya nane ya VPL.

Makosa ya beki wa pembeni Edward Charles yaliigharimu Yanga baada mchezaji huyo wa zamani wa JKT Ruvu kunyang'anywa mpira na winga huyo wa zamani wa mabingwa wa Uganda, KCCA FC.

Bao hilo lilidumu kwa dakika moja tu kwani katika dakika ya saba mfungaji bora wa VPL msimu uliopita Mrundi Amisi Tambwe aliyetemwa Simba na kujiunga na Yanga dirisha dogo, aliisawazishia timu yake mpya akimalizia kwa kichwa kikali krosi ya winga hatari Simon Msuva iliyopenyezwa ndani ya sita na kumwacha kipa Mwadin Ali wa Azam asijue la lufanya.

Lilikuwa bao la pili la Tambwe msimu huu katika mechi saba kati ya nane alizopangwa. Alifunga bao katika mechi ya Simba ya sare ya 2-2 dhidi ya Coatal Union Septemba 21 kwenye Uwanja wa Taifa. Tambwe hakupangwa katika kikosi cha Mzambia Patrick Phiri katika mechi ya suluhu dhidi ya Yanga. Kavumbagu amefikisha mabao matano msimu huu.

Katika kipindi cha kwanza, Azam ndiyo walicheza vizuri zaidi wakipata kona nne dhidi ya mbili za Yanga. Yanga walicheza rafu mara 11 dhidi ya nane za wageni wao, mashuti 5-5, kuotea 2-0 (Kpah Sherman dk 5 na Tambwe dk 33). Hapakuwa na kadi katika kipindi cha kwanza.

Dan Mrwanda aliyejiunga na Yanga akitokea Polisi Morogoro, alikuwa na nafasi nzuri ya kuifungia Yanga bao la pili lakini shuti lake la nje ya boksi lilipanguliwa kishujaa na kipa Mwadin na kuzaa kona dakika moja kabla ya mapumziko. Hadi mapumziko matokeo yalikuwa ni 1-1.

Yanga walikianza kwa kasi kipindi cha pili na kufanikiwa kupata bao la pili kupitia kwa Msuva aliyemchambua kwa kichwa kipa Mwadin baada ya kupenyezewa krosi na kiungo wa kimataifa Mrwanda Haruna Niyonzima katika dakika 53.

Mtokeabenchini John Bocco 'Adebayor' aliyeingia dakika ya 65 kuchukua nafasi ya kiungo mshambuliaji Salum Abubakar 'Sure Boy, aliisawazishia kwa kichwa murua Azam katika dakika ya 66 akiitendea haki krosi ya Erasto Nyoni ukiwa ni mpira wake wa kwanza kuugusa tangu aiingie uwanjani.

Idda Mushi anaripoti kutoka Morogoro kuwa katika mechi nyingine za VPL jana, timu ya Polisi Morogoro ilipata ushindi mzuri wa 2-0 dhidi ya Mgambo Shooting kupitia magoli ya Nicholaus Kabipe (dk.22) na Iman Mapunda (dk.85) aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kona iliyochongwa na Kabipe.

Nayo, Mbeya City ilipata ushindi wa 1-0 dhidi ya Ndanda FC, mfungaji akiwa ni Paul Nonga katika uwanja uliojaa maji kutokana na mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha.

Vikosi kwenye Uwanja wa Taifa vilikuwa; Yanga: Deogratius Munishi, Juma Abdul, Edward Charles/ Oscar Joshua dk.46, Mbuyu Twite, Kelvin Yondani, Salim Telela, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amisi Tambwe/ Mrisho Ngasa dk.83, Kpah Sherman na Dan Mrwanda/ Hussein Javu (dk.73).

Azam FC: Mwadin Ali, Himid Mao/ David Mwantika dk.90, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Mudathir Yahya, Salum Abubakar/ John Bocco dk.65, Didier Kavumbagu, Kipre Tchetche/ Amri Kiemba dk.53 na Brian Majwega.

Post a Comment

 
Top