Kocha wa Kagera Sugar, Jackson Mayanja amesema waliingia katika mechi
dhidi ya Simba wakiwa na dhamira ya ushindi (siyo kujilinda) na ameanika
sababu za kupata matokeo waliyoyataka baada ya kukizidi ujanja kikosi
cha Mzambia Patrick Phiri.Kagera Sugar iliibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya raundi ya nane ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Ijumaa na kuwa timu pekee iliyokusanya pointi sita kutoka kwa Simba na Yanga katika mechi za mzunguko wa kwanza msimu huu.
Katika mahojiano na NIPASHE mwishoni mwa wiki, Mayanja raia wa Uganda alisema: "Tulikuwa na uwezo wa kuifunga Simba mabao zaidi ya mawili lakini uchovu wa safari kutoka Kagera hadi Dar es Salaam na hali ya joto wakati wa mechi ilichangia timu yangu kutotengeneza nafasi nyingi za mabao. Tulipata nafasi mbili tukatumia moja."
"Tuliizidi Simba kimbinu ndiyo maana haikuweza kufanya mashambulizi ya hatari langoni kwetu. Tunaiheshimu Simba kwa sababu ni timu ngumu, lakini tulijipanga tukaja na mbinu za kupata ushindi. Tumefanikiwa na tunasonga mbele," alisema zaidi kocha huyo.
Kabla ya kuivaa Simba, Kagera Sugar walisafiri kwa siku mbili kwa basi dogo aina ya Toyota Costa kutoka Bukoba, Kagera hadi Dar es Salaam wakati Simba ilikuwa imeweka kambi Visiwani Zanzibar na ilitua kwa ndege jijini Ijumaa asabuhi kabla ya kushuka uwanjani jioni.
Kipigo hicho kilikuwa kibaya zaidi kwa nahodha wa Simba, Mganda Emmanuel Okwi na beki mpya mpya Kessy Ramadhani kwani kiliharibu siku yao ya kuzaliwa.
Mayanja alisema alijua wangeifunga Simba katika mechi hiyo, huku akisema Wekundu wa Msimbazi walifanya makosa makubwa kumtema mfungaji bora wa ligi hiyo msimu uliopita, Amisi Tambwe.
Simba ilimuacha Tambwe katika dirisha dogo la usajili, jambo ambalo Mayanja alisema Wekundu hao wanaweza kulijutia.
"Tulijua tutaifunga Simba, kwa sababu anayejua kupachika mabao
wamemuacha kwenye usajili wa dirisha dogo. Tambwe anatisha anapoingia kwenye 18. Kama wangekuwa naye wangekuwa nafasi kubwa ya kusawazisha na hata kushinda dhidi yetu," alisema Mayanja.
Post a Comment