Kutokana na hali hiyo, abiria hao wanalazimika kutumia muda mrefu kuzunguka kwa barabara kutokana na kukosa usafiri mbadala wa meli.
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, aliyekagua kivuko hicho jana, alisema meli hiyo ni ‘kimeo’ na itasimama kutoa huduma kwa miezi mitatu ikisubiri kufanyiwa ukarabati.
Akizungumza baada ya kuikagua alisema zinasubiriwa fedha toka Hazina ili meli iweze kukarabatiwa injini zake kisha iendelee na safari zake kama kawaida.
“Kwa sasa inatafutwa meli mbadala itakayosimama badala ya Mv. Victoria, lakini Mv. Serengeti inafanyiwa ukarabati ili iweze kutoa huduma kati ya Mwanza na Bukoba kwa kipindi hiki,” alisema Dk. Mwakyembe.
Alisema Mv Serengeti baada ya kukamilika kwake itakuwa ikibeba abiria mara tatu kwa wiki ili kupunguza tatizo la usafiri kwa wananchi wa maeneo hayo mawili ambao kwa sasa wanatumia usafiri wa barabara.
Aidha, Dk. Mwakyembe alisema ifikapo mwaka 2016, serikali itanunua meli iendayo kasi yenye uwezo wa kubeba abiria 50 na kusafiri siku moja kati ya Mwanza na Bukoba.
Awali Kaimu meneja mkuu wa kampuni ya meli nchini, Fabian Mayenga, alisema baada ya kuona meli Mv. Victoria ina upungufu, waliamua kuisimamisha ili kuepusha maafa yanayoweza kutokea kama yaliyotokea kwa Mv. Bukoba.
“Kwa sasa tunashughulikia Mv. Serengeti ili iweze kubeba abiria wa safari za Mwanza na Bukoba, matengenezo yanaendelea kwa sasa,” alisema Mayenga.
Alisema meli hiyo imezuiwa na mamlaka ya udhibiti usafiri wa nchi kavu na majini (Sumatra), baada ya kuwapo na kasoro mbalimbali kutokana na kushuka kwa msukumo katika mzunguko wa mafuta.
Katika hatua nyingine, Dk. Mwakyembe alisema serikali haitafufua Shirika la Ndege la ATC hadi pale itakapohakiki deni la Sh. bil.140 huku deni halisi lililopatikana likiwa ni Sh. bil. 90.
“Tutaendelea kuhakiki hadi itapofika Sh.bil.30, ndipo hapo tutakapolipa na kulifufua shirika hilo,” alisema Mwakyembe alipotembelea uwanja wa ndege wa Mwanza uliogharimu Sh. bil.100 katika matengenezo yake, zikiwamo Sh. bil.20 toka kwa hisani.
Post a Comment