0
Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe amepokea mabehewa 50 ya kubebea mizigo na mengine 22 kwa ajili ya abiria.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Dk. Mwakyembe alisema kupokelewa kwa mabehewa kumefanya idadi kufikia 100 kati ya 274.

Alisema ifikapo mwakani kutakuwa na mabadiliko makubwa katika njia ya reli ya kati kwani tayari wameshaanza kukifanyia kazi suala hilo ikiwa ni sehemu ya kuimarisha usafiri huo nchini.

Alisema mbali na mabehewa hayo kuna vifaa vingine vitawasili hivi karibuni hapa nchini na vichwa vipya 13 vya treni ambavyo vitasaidia kuongeza kasi ya utendaji kazi.

Dk.Mwakyembe alisema usafiri wa treni utakapoimarishwa kampuni ya Reli nchini (TRL) itaanza kujiendesha bila kutegemea fedha toka serikalini.

Aliongeza kuwa idadi ya mabehewa 274 yanaletwa kutoka Korea ya kusini na yamegharimu zaidi ya Sh. bilion 200.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Mhandisi Kipallo Kisamfu alisema mabehewa hayo yanatarajia kuanza safari zake kwa abiria ifikapo Januari mwakani na kwamba itakuwa ikielekea mikoa ya Kigoma na Mwanza.

Alisema kupokelewa kwa mabehewa hayo kutaongeza uwezo wa  kampuni katika kusafirisha mizigo kwa njia ya reli kwenda maeneo mbalimbali.

Post a Comment

 
Top