0
Kamati iliyoundwa kuchunguza uendeshaji na kuimarisha shughuli za Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), jana ilikabidhi taarifa ya uchunguzi jana jijini Dar es Salaam kwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe (pichani), na kumuomba kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa.

Kamati hiyo iliundwa na Waziri Mwakyembe baada kuwapo kwa malalamiko kutoka kwa wafanyakazi zikiwamo tuhuma mbalimbali.

Akizungumza mbele ya wafanyakazi wa kampuni hiyo katika mkutano ulioitishwa, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Malima Bundala, alisema kamati ilitembelea maeneo tofauti nchini, ili kukagua, kukusanya nyaraka pamoja na kufanya mahojiano kwa baadhi ya wafanyakazi.

Bundala alisema kati ya majukumu ambayo kamati hiyo ilipewa ni pamoja na kuangalia sera za kampuni, mishahara kwa wafanyakazi wa kima cha chini, tuhuma za viongozi na ubora wa mabehewa.

Kamati hiyo imependekeza kuwa mshahara ya wafanyakazi wa kima cha chini uwe ni Sh. 300,000 kwa mwezi, serikali kuharakisha utambuzi wa mali za TRL na RAHACO, uongozi kuhusisha wataalam katika kazi ya kutengeneza mabehewa pamoja na kampuni kuboresha uendeshaji wake ikiwamo mikataba ya wafanyakazi na mengineyo.

Waziri Mwakyembe baada ya kupokea taarifa hiyo alisema ndani ya siku tatu kuanzia jana atakutana na watendaji wa wizara yake kisha kukutana na wafanyakazi hao Desemba 6, mwaka huu, kwa ajili ya kutoa msimamo wa serikali.

“Taarifa hii ni ndefu naahidi yale ambayo yamependekezwa kwa lengo la kuboresha uendeshaji wa TRL, yatafanyiwa kazi. Nyinyi ni watu muhimu katika kutekeleza Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na tunatarajia kusafirisha tani milioni tatu kwenda bara,” alisema Waziri Mwakyembe.

Post a Comment

 
Top