Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen
Wasira amesema ubora wa mgombea ndiyo utakaokuwa msingi wa ushindi
katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Desemba 14 na Uchaguzi Mkuu 2015.
Akizungumza mjini Arusha mwishoni mwa wiki, Wasira
anayetajwa kuwa mmoja wa watu wanaowania kuteuliwa kugombea urais
kupitia CCM, alisema hakuna chama kitakachoshinda kwa kutegemea umaarufu
wake au wingi wa wanachama wake.
Alisema upigaji kura ungekuwa unazingatia chama,
basi CCM isingehangaika kupiga kampeni na kujinadi kwani ndicho chenye
wanachama wengi nchini na hivyo kingeshinda kirahisi.
Utafiti wa Twaweza
Akijibu swali la nini maoni yake kuhusu utafiti wa
Taasisi ya Twaweza kuhusu urais mwakani, Wasira alisema: “Kwanza
sijausoma utafiti wenyewe kujua vigezo na sampuli ya utafiti wao, lakini
lililodhahiri ni kwamba ubora wa mgombea au wagombea ndiyo msingi wa
ushindi kwenye uchaguzi.”
Waziri huyo aliyekuwa jijini Arusha kuhudhuria
vikao vya CCM kupitia nafasi yake ya ulezi wa chama hicho Mkoa wa Arusha
alisema kipindi cha viongozi kufikiria ukubwa na umaarufu wa vyama vyao
nyakati za kampeni na uchaguzi kimepitwa na wakati, badala yake kila
chama lazima kiwapime, kuwachuja na kupata wagombea bora.
“Ndani ya CCM tayari tumebaini hilo ndiyo maana
tuko makini kwenye uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali kuanzia
chaguzi za ndani na nje ya chama,” alisema.
Alisema CCM na viongozi wake wanaujua ukweli huo
kuwa wananchi hawaangalii itikadi zao za vyama wakati wa kupiga kura,
bali ubora wa mgombea. “Wananchi hawapigi kura kwa kuzingatia uanachama
wa vyama vyao. Hapana! Wanaangalia ubora wa mgombea. Mgombea bora
hushinda hata kama chama chake kina wanachama wachache katika eneo
husika,” alisema na kuongeza:
“Nawatoa hofu wanaCCM kuhusu uchaguzi wa Serikali
za Mitaa na Uchaguzi Ukuu mwakani. Chama kitasimamisha wagombea bora ili
kujihakikishia ushindi kama uchaguzi uliopita.”
Azungumzia Ukawa
Akijibu swali la iwapo CCM imeingiwa hofu ya
kushindwa kwenye chaguzi kuanzia Serikali za Mitaa baada ya vyama vikuu
vya upinzani nchini vya kuungana na kuunda Ukawa, Wasira alijibu kwa
kejeli akisema:
“Hakuna anayekatazwa kuota ndoto. Kuota ndoto ni
jambo la kawaida na kila mtu anaruhusiwa kuota. Ila ukweli unabaki kuwa
ndoto ni ndoto tu, ndiyo maana anayeota akiamka hutambua kuwa alikuwa
ndotoni.”
Post a Comment