0
UNICEF: Machafuko Nigeria yamewaathiri watotoWakati machafuko yakiendelea kushadidi Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, limetoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kuwasaidia watoto wanaokumbwa na masaibu makubwa nchini humo. Katika taarifa yake Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Anthony Lake amesema kuendelea kwa machafuko nchini humo kunaathiri watoto wasio na hatia akitolea mfano wa watoto, wanawake na vikongwe takribani 2,000 wameripotiwa kufanyiwa vitendo vya kinyama huko Baga.
Lake amesema kuwa kadhalika mtoto mwingine alifariki dunia baada ya bomu kumlipukia kifuani huko Maiduguri. Mkuu huyo wa UNICEF ameitaka jumuiya ya kimataifa kutosahau kuwa bado watoto zaidi ya 200 ambao walitekwa nyara na kundi la kigaidi la Boko Haram hawajapatikana. Lake amesema, maneno matupu hayatoshi kuelezea hasira dhidi ya vitendo hivyo wala kupunguza uchungu wa madhila hayo ya kaskazini mwa Nigeria na kusisitiza kuwa taswira za hivi karibuni nchini humo na athari zake kwa mustakabali wa taifa hilo zinahitaji hatua za haraka.

Post a Comment

 
Top