Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja.
Stori: Erick Evarist MBUNGE wa
Sengerema (CCM), William Ngeleja ameweka wazi kuwa pamoja na ushindani
kuwa mkubwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika hivi
karibuni, anajivunia ushindi mzito walioupata kupitia chama chake.
Uchaguzi huo ulifanyika nchi nzima Desemba 14, mwaka huu ambapo licha
ya kasoro ndogondogo zilizojitokeza katika baadhi ya maeneo na
kusababisha kurudiwa kwa mara ya pili, Desemba 21, CCM imeonesha kufanya
vizuri katika maeneo mengi.
Akizungumza na mwanahabari wetu, Ngeleja alisema anafahamu namna
ambavyo upinzani ulikuwa umejipanga kuhakikisha wanashinda lakini hakuna
jinsi inabidi wakubaliane na matokeo kwamba chama chake kimeibuka
kidedea katika jimbo lake.
“Katika jimbo langu la Sengerema, kwa vijini CCM tumepata ushindi wa
asilimia 85 wapinzani wakiambulia 15, vilevile katika vitongoji, CCM
tumepata asilimia 82 wao wamepata 18 hivyo hiyo ni ishara tosha kwamba
tunakubalika.
“Niwaahidi tu wakazi wa Sengerema kwamba hatutabweteka katika kazi
ambayo wametupa kuisimamia. Ilani yetu ni kuhakikisha tunaleta maendeleo
ya kila mwananchi wa jimbo letu na hata taifa kwa jumla,” alisema
Ngeleja.
Ngeleja alisema ana imani kabisa ushindi wa CCM hauishii katika ngazi
hiyo pekee bali hata ngazi za madiwani na wabunge hivyo wanaahidi
kusimamia ilani na ahadi ambazo walizitoa kwa wananchi wanazitekeleza.
Uchaguzi huo uliofanikiwa kwa kiasi kikubwa, ulisimamiwa na Ofisi ya
Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Post a Comment